Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Lazaro Nyalandu akizungumza katika mkutano uliohusisha wadau wa mashirika ya Kimataifa na asasi za kijamii ukiwa na lengo la ushirikishaji wa jamii katika masuala ya uhifadhi wa wanyamapori uliofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Mpingo House uliopo Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dar es Salaam.
Waziri Nyalandu akiendelea kutoa ufafanuzi.
Waziri Nyalandu akikazia jambo.
Naibu Waziri wa Maliaisli na Utalii, Mahmoud Mgimwa akitoa salamu kwa wadau wa taasisi za kirai. Kushoto Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Lazaro Nyalandu.
Mratibu wa Uhakiki wa
Ubora kutoka Haki Elimu, Robert Mihayo akitoa maoni kwa Waziri Mh.
Nyalandu ambapo amemuomba kushirikisha wadau wa elimu katika kutoa elimu
ya uhifadhi wa wanyamapori kuanzia ngazi ya elimu ya msingi ili
kuwaanda vijana ambao ni taifa la kesho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society, Francis Kiwanga akishiriki kutoa maoni katika masuala ya uhifadhi wa wanyamapori pamoja na kutokemeza ujangili wa Tembo.
Mwandishi wa gazeti la Daily News, Diriham Kimathi akiuliza swali kwa Waziri Nyalandu (hayupo pichani).
Wadau kutoka asasi za
kijamii na mashirika ya kimataifa waliohudhuria mkutano ulioitishwa na
Waziri Nyalandu ambao umefanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa
Mpingo House uliopo ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
...wakisikiliza kwa makini.
Waziri Nyalandu akisalimiana na baadhi ya wadau kutoka mashirika ya kimataifa na asasi za kijamii waliohudhuria mkutano huo.
Mdau kutoka Tanzania
Association on Climate Change, Ali Said Mosee akitoa maoni yake juu ya
kuhusiana na nini kifanyike katika masuala ya uhifadhi wa wanyamapori
katika mkutano uliotishwa na Waziri Nyalandu (hayupo pichani).
WAZIRI wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu amesema kama watanzania wasiposhirikiana katika
kudhibiti ujangili wa Tembo waliopo watatoweka kabisa katika kipindi cha
miaka 10 ijayo.
Kauli hiyo ameitoa jana
kwenye mkutano wa ushirikishwaji wa jamii katika masuala ya uhifadhi wa
wanyamapori uliofanyika wizarani kwake.
“Uhifadhi kama tunavyoujua, hautaweza kufanikiwa kama kila mtu kwenye nchi hii atafikiria ni kazi ya serikali kuu peke yake.
Na vilevile kama kila mtu atafikiria ni kazi ya wahifadhi peke yao”. alisema Nyalandu kwenye mkutano huo.
Nyalandu alibainisha
kuwa, majadiliano hayo, yatakuwa chachu kubwa ya maendeleo katika wizara
hiyo huku akiwashukuru wadau hao mbalimbali wakiwemo wanahabari kwa
kufika kwao, ili kuangalia suala la uhifadhi kwa mapana yake.
Alisema wakati ujangili
wa Tembo nchini umeshamiri sana, wakati umefika kwa watanzania
kuhakikisha kwamba wanakomesha hali hiyo ili taifa kuendelea kuwa na
wanyama wake.
Alisema mathalani Tembo
katika hifadhi ya Selous wamepungua kutoka Tembo 38,975 katika sensa ya
mwaka 2009 hadi Tembo 1,384 kwa sensa ya mwaka 2014 na akasema kwa kasi
hiyo katika miaka 10 ijayo Tembo Tanzania wataisha kabisa.
“Hili ni muhimu watu
wakafahamu, upana wa hivi vita ni mkubwa kiasi gani na watu wanaohusika
ni wengi kiasi gani ndani na nje ya nchi," alisema Nyalandu akiongeza
kuwa mitandao ya kihalifu imetanda ulimwenguni kote.
Alisema suala la hifadhi halipo kwa wanyama pekee bali lipo katika upana wote na hata katika misitu.
Alisema ili kukabiliana
na ukatwaji hovyo wa miti kutoka katika misitu ya miombo wanajipanga
kuhakikisha kwamba miombo inayodaiwa kuingizwa nchini kutoka Zambia
inakamatwa ili kulinda miombo iliyopo magharibi ya nchi.
Akizungumzia suala la
mifugo na mbuga zinazopakana nazo amesema kwamba wanaanda rasimu ya
kuhakikisha kwamba kuna mahusiano mazuri kati ya wenye mifugo na hifadhi
wakiwa tayari kuyaachia baadhi ya maeneo kwa lengo la kuhakikisha
kwamba wafugaji hawaingizi mifugo yao katika hifadhi.
Aidha amesema kwamba
wanajipanga namna ya kuhakikisha kwamba hakuna mgongano wa maeneo kati
ya wanyama na binadamu na kwamba wanavijiji wanafundishwa namna ya
kuishi na wanyama katika maeneo yenye mwingiliano mkubwa.
Aidha alisema kwamba
meno ya Tembo kilo 1,763 yalikamatwa mwaka jana na jitihada zinaendelea
za kukabiliana na majangili kwa kutanua mtandao wa kiintelejensia ndani
na nje.
Alisema kwa sasa
wanamsaka raia wa China anayeshutumiwa kutorosha nyara za serikali kwa
kushirikiana na jeshi la Polisi la Kimataifa (Interpol).
Kwa nje ya nchi, meno ya Tembo yaliyokamatwa, Kilo 40 katika miji ya Hong Kong, China.
Aidha alisema watuhumiwa
1,711, walikamatwa kuanzia Januari hadi Desemba mwaka jana na kesi zao
zinaendelea katika mahakama mbalimbali hapa nchini. Pia silaha 85
zimekamatwa ikiwemo silaha za kivita ambazo walikuwa wakizitumia
mbugani.
Alisema ukichanganya na silaha zilizokamatwa kwenye operesheni tokomeza, jumla silaha 1,199 zimekamatwa.
Kwa upande wake, Ali
Said Mosee aliyehudhuria mkutano huo kutoka Tanzania Association on
Climate Change, alishauri ushirikishaji wa wadau mbalimbali kutatua
migogoro kwenye mipaka ya mbuga na pia mgongano wa kimaslahi kati ya
hifadhi na wanadamu.
Aidha wadau walishauri
Wizara kuhakikisha inapunguza misafara ya wanyama ya kuhamahama kutoka
sehemu moja hadi nyingine ikiwemo kwa kuzalisha miti na mazao
yanayopendwa na wanyama hao.
“Wanyama wetu wanatakiwa
wafanyiwe utafiti na kujua nini Nyati anapendelea kula porini, basi
wapande hiyo miti na vyakula vyake kwa ujumla hata kwa Tembo hivyo
hivyo.Wapande hiyo miti hapa hapa kwani hata siye binadamu
tunavyovyakula tunavyovipenda, naamini hata kwa wanyama ni hivyo hivyo,
rai yangu ni kuwa tufanye utafiti na kujua ili kuzuia misafara hii”
alisema Ali Said Mosee.
Tanzania inahifadhi za
taifa 16 na asilimia 40 ya ardhi ya nchi ni maeneo yaliyohifadhiwa. Kati
ya maeneo hayo yaliyohifadhiwa hadi mwezi uliopita mwaka huu 2015,
maeneo 19 yanamilikiwa na wananchi na yameshasajiliwa. Pia alisema
kwamba kuna mapori ya akiba, 28 nchi nzima.
“Watu wengi wanadhani
kwamba misitu yote inamilikiwa na serikali kuu. Ukweli ni kwamba
serikali kuu inamiliki asilimia 35 tu ya misitu ya nchi yetu, misitu
mingine yote inamilikiwa na vijiji, wilaya na watu binafsi asilimia 7. "
alibainisha waziri huyo.
Aliwataka watendaji wa
Serikali za mitaa kukabiliana na changamoto ya kutoweka kwa kasi kwa
misitu ili taifa lisitumbukie katika jangwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni