Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi akiwa kwenye picha ya pamoja na ujumbe
wa Tanzania na wajumbe toka nchi wanachama wa WMO.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
Dkt. Agnes Kijazi pamoja na ujumbe wa Tanzania akiwemo Bwana Mohamed Ngwali,
Mkurugenzi wa TMA – Ofisi ya Zanzibar, wanashiriki mkutano mkuu wa 17 wa Shirika
la Hali ya Hewa Duniani (WMO) unaofanyika Uswisi, makao makuu ya Shirika hilo
kuanzia tarehe 25 Mei hadi 12 Juni 2015.
Akizungumzia umuhimu wa mkutano huyo, katika
mahojiano yaliyofanyika kabla ya kuanza safari
Dkt. Kijazi alisema ni muhimu kwa Tanzania kushiriki mkutano huo ili
kutekeleza makubaliano ya kimataifa.
Aliongeza kusema mkutano huo ni wa 17 na utahusisha uchaguzi na
uthibitisho wa Katibu Mkuu wa WMO, uchaguzi wa Rais wa WMO na makamu wake
watatu pamoja na uchaguzi wa wajumbe wa Baraza kuu (Executive Council).
Aidha
Dkt. Kijazi alisema mkutano huo utapitia na kupitisha mipango ya muda mrefu na
bajeti ya shirika hilo. ‘ Tanzania itahusika moja kwa moja katika uchaguzi wa
Katibu Mkuu, Rais, Makamu wa Rais na wajumbe wa baraza kuu pamoja na kupitisha bajeti na mpango
mkakati wa muda mrefu kwa ajili ya shirika hilo’ Alisema Dkt. Kijazi.
Shirika hilo limekuwa likifanya mkutano mkuu kila
baada ya miaka minne (4) na kushirikisha nchi wanachama ambao kwa sasa idadi
yake ni 191.Kwa kipindi cha hivi karibuni dunia imekuwa
ikikabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa, hivyo moja ya agenda
ni kuhakikisha mkutano huo unaweka mikakati yenye tija katika kupambana na
changamoto hizo sambamba na ajenda nyingine mbalimbali zitakazojadiliwa.
Tunawatakia Dkt. Kijazi na Ujumbe wote wa Tanzania
majadiliano yenye tija katika mkutano huo muhimu.
IMETOLEWA NA: MONICA MUTONI,
OFISA MAHUSIANO MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni