Wazee wanaoishi katika mazingira magumu jijini Mwanza wakiomba msaada kutoka kwa wasamaria wema kandokando ya mzunguko waMnara wa Mashujaa.
Kwa ufupi
Baadhi ya mikoa inayotoa ombaomba kwenda Dar es Salaam ni Singida, Lindi, Tanga , Kigoma, Mbeya na Mwanza
Kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la FHI360, linashughulika na masuala ya Familia na Afya chini ya mradi wa Pamoja Tuwalee uliofanyika mwaka 2013, kati ya watoto 332 ombaomba waliohojiwa, asilimia 35.5 sawa na watoto 118, wanatoka mkoani Dodoma.
Asilimia 13.6 wanatoka mkoani Dar es Salaam na Mtwara inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na asilimia 3.3.
Dodoma. Si kila ombaomba aliye katika mitaa ya jijini Dar es Salaam au majiji na miji mingine nchini anatoka mkoani Dodoma.Hata hivyo, ipo dhana katika fikra za walio wengi kuwa daima ombaomba hutokea mkoani Dodoma, jambo ambalo limedhihirika kuwa halina ukweli, ingawa ni ukweli usiopingika kuwa wengi hutoka katika baadhi ya vijiji vilivyo kwenye mwambao wa reli ya kati mkoani humo.Sababu za hali hiyo zinatajwa kuwa ni za kimazingira ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa wananchi wa maaneo hayo kuwa maskini, lakini nyingine inaelezwa ni hulka ya watu wengi katika maeneo hayo kutopenda kufanya kazi ngumu hasa kilimo hivyo kuwa ombaomba.Makala haya hayalengi kuwazungumzia ombaomba, bali maisha na changamoto za Hamisi Peter (44), mlemavu wa viungo ambaye amekimbiwa na mkewe baada ya kupata ajali na kuthibitika kwamba atakuwa akiishi maisha ya ulemavu.Pia lengo si kuelezea tukio la Peter kukimbiwa na mkewe, bali maelezo yake kwamba hapendi na anachukia maisha ya kuombaomba.“Mimi sipendi maisha haya ya kuombaomba, mwili wangu unanilazimisha niishi hivi. Napenda nitoke katika maisha haya ya aibu na manyanyaso makubwa. Nafsi yangu haifurahii maisha haya yasiyokuwa na heshima, lakini nitafanya nini wakati watoto wawili wananitazama mimi na mama yangu ambaye ni kikogwe pia ananitazama mimi? Sina namna zaidi ya kuomba,” anasema Peter na kusisitiza:“Ndiyo hivyo tena, ‘roho ipo radhi, lakini mwili ni dhaifu’, sina budi kuishi kwa kuombaomba ili kunusuru maisha yangu na watoto wawili waliotelekezewa na mke wangu.”Anasema hawezi kuusahau mwaka 2011 kwani ndiyo uliobadili maisha yake na kuyaweka katika mitazamo mitatu.“Nilijishughulisha na kazi halali za kuniingizia kipato, lakini sasa ni ombaomba, pili; mwaka 2011 uliweka alama ya mwisho wa uhusiano wa ndoa kati yangu na mke wangu, tatu; ni mwaka uliogharimu viungo vyangu na sasa wananiita ‘Hamisi mlemavu,” anasema.Anasema kuwa mwaka huo akiwa mkoani Morogoro akifanya kazi ya kuuza nyama katika bucha lililomilikiwa na Hassan Idd, siku moja alfajiri wakati wakienda machinjioni, gari walilotumia lilipata ajali iliyogharimu maisha ya wenzake wawili, huku yeye akiachiwa ulemavu.Anasimulia kuwa baada ya ajali hiyo, alijikuta akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro ambako kutokana na hali yake ilivyokuwa, wataalamu katika hospitali hiyo walishauri apelekwe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), KCMC au Hospitali ya Mkoa ya Dodoma (General Hospital) kwani huko kuna wataalamu wa mifupa waliobobea.Kutokana na ushauri huo, Peter anasema aliamua kwenda Hospitali ya Dodoma kwa kuwa ni jirani na nyumbani kwao akiamini ingekuwa rahisi kupata hata huduma nyingine. Hakika, akiwa hospitalini hapo alihudumiwa ipasavyo akapona, ingawa amebaki akiwa mlemavu wa viungo kutokana na nyoga na mguu wa kulia kuthibitika kuwa viliathirika zaidi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni