Social Icons

Jumamosi, 16 Mei 2015

Hakika Rais Kikwete Amefanya Uamuzi Sahihi

 

Juzi, Rais Jakaya Kikwete aliiagiza Manispaa ya Kinondoni iondoe maji yaliyozingira nyumba za watu mara moja wakati ikitafakari mipango ya muda mrefu ya kukabiliana na mafuriko ya maji jijini Dar es Salaam, ambayo kwa kiasi fulani pia husababishwa na mitaro kujaa uchafu.


Rais Kikwete alitoa agizo kama hili siku chache wakati alipotembelea eneo la Jangwani na kukuta tatizo kama hilo la nyumba kuzungukwa na maji na hivyo kusababisha wakazi wengi kushindwa kuendelea na shughuli zao za kujipatia riziki kutokana na adha hiyo.



Akitoa agizo hilo, Rais alisema kuwa wahandisi wanajua watawezaje kuondoa maji hiyo kwa kutumia taaluma yao na kwamba maisha lazima yaendelee na baada ya kuyaondoa ndipo wakae kuangalia ni jinsi gani watajenga mifereji ili kupunguza ukubwa wa tatizo hilo.


Tunapenda kumpongeza Rais Kikwete kwa uamuzi huo, ambao umezingatia kutatua matatizo yanayowakabili wananchi sasa pia kuangalia baadaye hali hiyo itadhibitiwa vipi.


Huu ni uamuzi ambao wananchi wangependa kuusikia kwenye matatizo mengine mengi yanayowakumba kila wakati. Mara nyingi viongozi wa kisiasa hupenda kueleza mikakati mingi mikubwa na ya muda mrefu wakati kunapotokea tatizo linalohitaji utatuzi wa haraka.



Wakati mvua zilipopamba moto na mafuriko kukumba sehemu nyingi za Jiji la Dar es Salaam, mamlaka ziliibuka na mpango mkubwa wa kuliboresha Jiji la Dar es Salaam ambao unahitaji mabilioni ya fedha kuufanikisha.


Hizi hazikuwa habari ambazo wananchi wangetaka kuzisikia wakati wakiwa katikati ya matatizo makubwa ya mafuriko, ambayo yalisababisha barabara nyingi kufungwa na hivyo kusababisha misururu mikubwa ya magari nyakati zote, hali ambayo kwa kiasi kikubwa iliathiri utendaji kwenye ofisi nyingi na kuathiri kipato cha wafanyabiashara, hasa ndogondogo.



Wakati huo, wananchi walitarajia kusikia mamlaka zimejipangaje kuhakikisha adha wanayopata kutokana na mvua hiyo inapunguzwa kwa kuchukuliwa kwa uamuzi wa haraka. Wananchi wanajua fika kuwa mvua kubwa kama hizo hutokea wakati wowote bila ya binadamu kuweza kuzizuia, lakini wanajua kuwa athari na kero zake zinaweza kupunguzwa kwa kuwa na viongozi walio tayari kufanya hivyo.


Ndiyo maana Rais Kikwete ameliona hilo na kuziagiza mamlaka husika kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha maji hayo yanaelekezwa yanakotakiwa kwenda kwa kuwa mafuriko hayo pia yamechangiwa na shughuli za binadamu.



Kwa sasa, Jiji la Dar es Salaam linakabiliwa na tatizo kubwa la foleni za magari na hakuna shaka kwamba tatizo hili linaathiri kwa kiasi kikubwa mapato ya mamlaka za jiji na wilaya zake, kutokana na ofisi nyingi na biashara kutofanya kazi kwa kiwango chake.



Utatuzi wa tatizo hili unaelezewa kwa mikakati mikubwa ya muda mrefu, wakati hali inazidi kuwa mbaya kadri siku zinavyokwenda. Hivi wahusika wanataka hadi hiyo miradi ikamilike ndipo tatizo hili liishe, au wanaweza kuchukua hatua za makusudi kupunguza tatizo hili?


Tunaamini kwamba kama mamlaka za jiji zitakaa na kutafakari njia za kupunguza tatizo hili kwa sasa wakati miradi mikubwa ikishughulikiwa, tatizo hili litapungua na wakazi wataondokana na adha hii wakati wakisubiri hali nzuri zaidi baadaye.


Uamuzi wa Rais Kikwete kuwataka wahusika Kinondoni na Ilala kutafuta suluhisho la muda la tatizo la mafuriko, pia uwazindue katika kufikiria jinsi ya kupata suluhisho la muda la matatizo mengine mengi kama hili la misururu ya magari.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni