Tatizo la unywaji pombe
wa kupindukia kwa wanaume wilayani hapa, limechukua sura mpya baada ya
jeshi la polisi mkoa wa Kilimanjaro kutuhumiwa kushiriki kuchochea
biashara hiyo.
Akiongea katika mkutano
wa hadhara kuhusu tatizo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas
Gama, alisema kuwa taarifa mbali mbali zinaonyesha kuwa baadhi ya askari
si waaminifu katika vita dhidi ya pombe haramu inayoendelea hivi sasa
wilayani humo.
“OCD taarifa zinaonyesha
kuna baadhi ya askari wako, ambao wanashirikiana na wafanyabiashara wa
pombe haramu ya gongo na hili linafanya kazi ya operesheni kukomesha
tabia hii mbaya kuwa ngumu,” alisema.
Alisema taarifa hizo
zikiwamo zile za kutoka kwa wananchi wenye nia njema na vita hiyo,
zinaonyesha kuwa baadhi ya askari wasio waaminifu wamewageuza
wafanyabiashara wa gongo kuwa ATM zao (mashine za kutolea pesa) kwa
kuchukua rushwa hivyo kusababisha uovu huo uendelee.
Gama alisema serikali
haijamzuia mtu kunywa pombe halali ili mradi isiwe ni wakati wa kazi na
kwamba pale itakapobainika kuna wanao kunywa wakati wa saa za kazi
watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.
“Inasikitisha kusikia
kuwa baadhi ya pombe zinazonyweka Rombo zimetengenezwa na mbolea aina ya
urea, maji ya betri, spiriti, kinyesi cha binadamu, sukari guru na
molasesi, hii ni hatari kwa afya ya mwanadamu,” alisema.
Kwa upande wake Padri
Serafini Kilawe, wa Kanisa Katoliki, alisema kuwa vita dhidi ya pombe
haramu hasa ya gongo haitaweza kumalizika iwapo baadhi ya askari
hawataacha kushirikiana na wanaotengeneza pombe hizo.
Suala la ulevi
uliokithiri limekuwa gumzo maeneo mbali mbali mkoani Kilimanjaro na nje
ya mkoa huo, ambapo imedaiwa kuwa baadhi ya wanawake wilayani humo
wanalazimika kukodi wanaume kutoka nchi jirani ya Kenya ili kukidhi
mahitaji yao ya kindoa.
Wananchi waishio
wilayani hapo, Elizabeth Shabani na Mary Shirima, walikiri kuwapo kwa
askari, wanaofika maeneo wanapotengenezea pombe haramu kuchukua fedha
kila mwisho wa mwezi kama ni ujira wa kuwalinda.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni