Baadhi ya wazazi wa shule ya msingi Kilimani waliohudhuria kwenye
mkutano wa wazazi wa shule hiyo uliofanyika kwenye viwanja vilivyotengwa
kwa ajili ya mikutano shuleni hapo.(Picha zote na Jumbe Ismailly).
WANAFUNZI 365 pamoja na walimu wanane wa shule ya msingi Kilimani,
kata ya Ibaga, tarafa ya Kirumi, wilayani Mkalama wanachangia matundu
manane ya choo yaliyopo kati ya matundu 17 yanayohitajika katika shule
hiyo.
Hayo yalibainishwa na mwalimu mkuu wa shule hiyo, Hamisi Masimba
kwenye mkutano wa wazazi wa shule hiyo uliofanyika kwenye viwanja
vilivyotengwa kwa ajili ya kufanyia mikutano mbali mbali ya shule hiyo.
Aidha mwalimu huyo alifafanua kuwa kutokana na upungufu huo wa
matundu ya choo yaliyotenganishwa sehemu ya wanafunzi wa kiume na wa
kike na ukuta,kumechangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi wa kiume na wa
kike wanapojisaidia huanza kuchunguliana kwenye matundu yaliyopo ili
kuangalia anachofanya mwenzake.
Hata hivyo kibaya zaidi katika matumizi ya huduma hiyo shuleni hapo
ni kwamba inapofikia wakati mwalimu yeyote yule anapotaka kwenda
kujisaidia kwenye vyoo hivyo hulazimika kuweka ulinzi wa mwalimu
mwenzake nje kuwazuia wanafunzi kwenda kujisaidia kwa wakati huo,
kitendo ambacho kinaweza kuchangia wanafunzi kujisaidia kwenye eneo la
msitu uliopandwa karibu na shule hiyo na hivyo hatarisha mazingira ya
shule.
“Kwa kweli hali ya matundu ya vyoo katika shule yetu hii ni ya
kutisha kwani kutokana na wanafunzi wote kutumia jengo moja lenye
matundu ya vyoo manane lililotenganishwa na ukuta tu na hivyo
wanapokwenda kujisaidia huanza kuchunguliana kila mmoja aweze kumuona
mwenzake anavyojisaidia”alisisitiza mwalimu huyo.
Kwa mujibu wa Masimba katika mkutano huo uliolenga kuwahamasisha
wazazi kuchangia chakula cha mchana kwa watoto wao baada ya WFP kuanza
kukaribia kumaliza kipindi chake cha kutoa msaada,alisema ili kuondokana
na adha hiyo wamelazimika kuwaita wazazi ili kuwaomba wachangie ujenzi
wa matundu hayo kupunguza na kama siyo kumaliza tatizo hilo.
Hata hivyo wakati mkutano huo wa wazazi ukiendelea mwandishi wa
habari hizi alishuhudia wanafunzi wa kiume na wale wa kike wakifukuzana
kuwahi kwenda kujisaidia kabla ya mwingine,na hivyo kutokana na uhaba
huo wa matundu walilazimika kulundikana kwenye milango wakisubiriana
kuingia.
Baada ya kamati ya shule kujenga hoja kwa wazazi kuhusu tatizo hilo
ndipo wazazi walikubaliana kuchangia shilingi mia tano kila kaya kwa
ajili ya kumlipa fundi atakayefukua shimo la choo lenye matundu mawili
na kukamilisha ujenzi wake kabla ya mwisho wa mwezi huu matundu hayo
yawe yamekamilika.
Changamoto zingine zinazoikabili shule hiyo inayoongoza kwa
kufaulisha wanafunzi wote wa darasa la saba kuanzia mwaka 2012 hadi 2014
ni pamoja na upungufu wa vyumba vya madarasa matatu kati ya vyumba tisa
vinavyohitajika,nyumba za walimu kumi zinazohitajika,ofisi mbili za
walimu kati ya tatu na stoo moja kati stoo mbili zinazohitajika.
Shule ya msingi Kilimani iliyofunguliwa aprili,08,2008 ikiwa na
darasa la kwanza hadi la tatu,huku ikiwa na walimu wawili na madarasa
mawili,hivi sasa shule hiyo ina jumla ya walimu wanane ina wanafunzi 365
wanaofundisha darasa la kwanza hadi la saba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni