Rais wa Burundi,Pierre Nkurunziza. PICHA|MAKTABA
Kwa ufupi
- Awali, kulikuwa na taarifa kuwa kiongozi wa uasi huo, Meja Jenerali Godefroid Niyombare alikuwa amekamatwa pamoja na wasaidizi wake, lakini baadaye mshauri wa habari wa rais, Willy Nyamwite alisema alipewa taarifa zisizo sahihi.
Dar/Mashirika. Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza amewasili jijini Bujumbura ikiwa ni siku mbili baada ya waasi kutangaza kumuondoa madarakani na tayari majenerali watatu waliotangaza mapinduzi wamekamatwa huku wanajeshi 12 wakiuawa.Awali, kulikuwa na taarifa kuwa kiongozi wa uasi huo, Meja Jenerali Godefroid Niyombare alikuwa amekamatwa pamoja na wasaidizi wake, lakini baadaye mshauri wa habari wa rais, Willy Nyamwite alisema alipewa taarifa zisizo sahihi.Lakini wakati kukiwa na habari kuwa Meja Jenerali Niyombire amekamatwa, waasi hao wamesema wataendeleza vita dhidi ya majeshi ya Serikali kwa ajili ya kumuondoa Rais huyo ambaye anapingwa kutokana na kutangaza kugombea urais kwa mara ya tatu kinyume na katiba.“Amekamatwa, alikataa kujisalimisha,” Gervais Abayeho, msemaji wa Rais Nkuruzinza aliliambia Shirika la Habari la Uingereza, Reuters.Msafara wa Rais Nkurunziza ulionyeshwa kwenye televisheni ukiwasili jijini Bujumbura, ingawa picha hizo hazikumuonyesha Rais huyo ambaye alipitia kijijini kwake Ngozi kabla ya kwenda jijini humo akitokea Tanzania.Mnadhimu wa Jeshi, Jenerali Prime Niyongabo, akizungumza kwa mara ya kwanza tangu majeshi yanayomtii Nkurunziza yadhibiti redio na televisheni ya serikali, alisema wanajeshi 12 wa upinzani waliuawa wakati wa mapambano ya kuwania kituo hicho juzi.Alisema wanajeshi wengine 35 wa uasi walijeruhiwa na 40 wamejisalimisha.Alisema wanajeshi wanne wa Nkurunziza walijeruhiwa.Hali ya jijini Bujumbura ilikuwa shwari jana baada ya mapambano kutawala siku nzima ya juzi wakati majeshi yanayomtii Nkurunziza yalipokuwa yakipambana kukomboa sehemu muhimu.“Tunatoa wito kwa wakazi wa Manispaa ya Bujumbura kufungua tena biashara zao. Hali sasa imesharejea kuwa ya kawaida baada ya kushindwa kwa waasi,” Meya wa Bujumbura, Saidi Juma aliliambia shirika la habari la China, Xinhua.Baada ya kuwasili, Rais Nkurunziza alipewa taarifa fupi ya mapinduzi na hata jinsi jeshi lilivyofanikiwa kuzima uasi na kutwaa tena miji ya Bujumbura.“Rais Pierre Nkurunziza sasa yuko Burundi,” Msemaji wa Serikali, Willy Nyamitwe alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni