Darry Rwegasira
SERIKALI imepokea tuhuma dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Darry
Rwegasira za madai ya kuwanyanyasa wananchi wa wilaya hiyo na kuwapa
kipaumbele wahamiaji haramu kutoka Rwanda.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri MKuu (Sera, Uratibu na Bunge),
Jenista Mhagama alisema hayo jana wakati akitoa kauli ya serikali kuhusu
tuhuma zilizotolewa na Mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes (CCM) katika
kikao cha bunge kinachoendelea.
“Hizi tuhuma sio za kupuuzia, ni tuhuma nzito, serikali tumelichukua
hilo na tunalifanyia kazi ili kupata ukweli wake ili hatua stahiki
zichukuliwe”, alisema Mhagama.
Awali akichangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa mwaka
2015/16, mbunge huyo alimtuhumu Mkuu huyo wa Wilaya kuwa ndiye
anayechochea mgogoro wa ardhi katika wilaya hiyo, kwa kuwanyanyasa
wananchi wa Karagwe na kuwapa kipaumbele wahamiaji haramu wa Rwanda.
“Migogoro mingi ya ardhi kwenye wilaya yetu inachangiwa na huyu mkuu
wa wilaya, kwanza kimwili yuko Tanzania lakini kiroho yuko Rwanda,
haiwezekani anawanyanyasa wananchi wa Tanzania kwenye ardhi yao na
kuwapa kipaumbele wahamiaji haramu wa Rwanda,” alihoji Blandes.
Kutokana na hali hiyo, Blandes alimuomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
kumshauri Rais Jakaya Kikwete kumwondoa mkuu huyo wa wilaya haraka
wilayani humo.
Hata hivyo, baada ya mbunge huyo (Blandes) kumaliza kuchangia hakuna
mtendaji wa serikali aliyejibu kauli hiyo, hadi kipindi cha uchangiaji
kilipokamilika mchana kwa Mbunge wa Viti Maalumu, Rosemary Kirigini
(CCM), kusimama na kuomba mwongozo kuhusu kauli hiyo.
“Mheshimiwa mwenyekiti, nimesimama hapa kwa Kanuni za Bunge ya 68(7)
inayosema Mbunge anaweza kusimama muda wowote kutolea ufafanuzi, jambo
lililojitokeza mapema wakati wa mjadala... sasa mheshimiwa mwenyekiti
kuna tuhuma nzito zimetolewa leo (jana) hapa na Mbunge Blandes dhidi ya
mkuu wa wilaya ya Karagwe,” alisema Kirigini.
Kirigini, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Meatu alisema: “Tujuavyo
sisi, Mkuu wa Wilaya ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Wilaya na
ni Mwakilishi wa Rais kule, lakini kauli iliyotolewa hapa mbele yako ni
ya uchochezi, sasa mheshimiwa mwenyekiti naomba mwongozo wako.”
Mara baada ya kumaliza, alisimama Mhagama na kusema: “Mheshimiwa
mwenyekiti sisi kama serikali tumelichukua hili na tutafanya uchunguzi
kuona alichokisema mheshimiwa (Blandes) na uhalisia na tutachukua
uamuzi.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni