Kiongozi wa chama cha upinzani cha FNL nchini Burundi Bw. Agathon Rwasa
Kiongozi wa chama cha upinzani cha FNL nchini Burundi amesema nchi hiyo
ya Afrika Mashariki inakaribia kutumbukia tena kwenye vita vya ndani na
ameitaka jamii ya kimataifa kuingilia kati ili suala hilo lisitokee.
Akizungumza kwenye mahojiano maalumu mapema hii leo, Agathon
Rwasa amesema jeshi la Burundi linaonekana kugawanyika baada ya tangazo
lililotolewa hapo jana na Jenerali Godefroid Niyombare, kwamba
ameipindua serikali ya Rais Pierre Nkurunziza.
Bw. Rwasa amesema iwapo mapinduzi ya kijeshi yanayoendelea yatakosa
kufanikiwa na Rais Nkurunziza akarudi madarakani na kudhibiti hali ya
mambo, kiongozi huyo atahitajika kutumia fursa hiyo kufungua milango ya
mazungumzo badala ya kutumia mkono wa chuma dhidi ya mahasimu wake.
Kiongozi wa chama cha FNL pia amesema iwapo mapinduzi yatafanikiwa,
wafanyamapinduzi watapaswa kujumuisha Warundi wote katika mchakato wa
kurudisha utawala wa sheria haraka iwezekanavyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni