Jumuiya ya
Kimataifa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York
imeelezea msimamo wake thabiti wa kuunga mkono kwa dhati na kwa kila
hali kazi na jukumu ya Jopo la Watu Mashuhuri Duniani la Kukabiliana na
Majanga Duniani linaloongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete (pichani).
Jumuiya
hiyo imeeleza msimamo wake wa kuunga mkono Jopo hilo wakati Rais Kikwete
na wana-Jopo wenzake walipopata nafasi ya kuwaelezea Wawakilishi wa
Kudumu wa nchi mbali mbali duniani katika Umoja wa Mataifa kuhusu kazi
iliyofanywa na Jopo hilo katika siku za mwanzo kabisa.
Jopo hilo
lililotangazwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Mheshimiwa Ban
Ki Moon Aprili 2, mwaka huu, limepewa jukumu ya kupendekeza jinsi gani
dunia inavyoweza kukabiliana na majanga ya kiafya duniani, na hasa
magonjwa ya milipuko, kama ilivyokuwa Ebola katika nchi za Afrika
Magharibi za Guinea, Liberia bna Sierra Leone.
Baada ya
wiki moja ya kazi kubwa mjini New York, Rais Kikwete na wajumbe wa Jopo
hilo kutoka Brazil, Botswana, Indonesia, Uswisi na Marekani, wamekutana
na Wawakilishi wa Kudumu wa mataifa mbali mbali katika UN kuwaelezea
nini kimefanyika na nini kinatarajia kufanyika.
Baada ya
maelezo ya wajumbe wa Jopo, mwakilishi wa Ubalozi wa Ujerumani katika UN
alisema kuwa Ujerumani inaunga mkono moja kwa moja kazi ya Jopo hilo
akisisitiza kuwa Kiongozi wa Ujerumani, Kansela Merkel amekubali kutoa
kiasi cha dola za Marekani milioni moja kuunga mkono shughuli za Jopo
hilo.
Mwakilishi
wa Senegal alisema kuwa nchi yake inaunga mkono moja kwa moja kazi ya
Jopo hilo lililoteuliwa na Katibu Mkuu wa UN, akisisitiza kuwa Senegal,
kama Mwenyekiti wa Kamati ya Oslo ya Afya katika Umoja wa Mataifa
itashirikiana na Jopo hilo moja kwa moja.
Mwakilishi
wa Ufaransa amesema kuwa nchi yake inaunga mkono kazi ya Jopo moja kwa
moja na kuwa ni uamuzi wa busara wa Katibu Mkuu wa UN kuunda Jopo hilo.
Mwakilishi
wa Uingereza amepokea kwa mikono miwili uundwaji wa Jopo hilo,
akisisitiza kuwa nchi hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada za Jopo hilo
kama ilivyoiunga mkono Sierra Leone wakati wa kukabiliana na Ebola.
Mwakilishi
waLuxembourg amesema kuwa dunia inalitarajia Jopo hilo kuelekeza nguvu
yake katika mapendekezo ya uongozi kuliko changamoto za kiufundi. Aidha,
ameongeza kuwa nchi hiyo baada ya kushika Uenyekiti wa Umoja wa Ulaya
(EU) itaongeza kazi yake katika kuchunguza athari za Ebola na kiini
chake.
Mwakilishi
wa Marekani amesema kuwa ni muhimu kwa Jopo kuweka msingi wake katika
ugonjwa wa Ebola lakini katika magonjwa mengine ya mlipuko ili kuweza
kupata uhakika zaidi wa athari za magonjwa hayo.
Naye, mwakilishi wa Uswisi amesema kuwa nchi yake inahitaji mapendekezo ya kisiasa kuliko yale ya kiufundi ama ya kimfumo. “Tunahitaji kazi kubwa ya kisiasa hapa kututoa katika matatizo ya sasa.”
Naye
Mwalikishi wa Misri amesema kuwa nchi yake inaheshimu sana uteuzi wa
Jopo hilo na kuamini kuwa Rais Kikwete ni kiongozi mwafaka katika
kukabiliana na majanga ya kiafya duniani.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
9 Mei, 2015
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni