Raia 60 wa Burundi wamesafirishwa kutoka Kituo cha Mapokezi cha Kasange wilayani Ngara mkoani Kagera na kupelekwa kwenye Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu wilayani Kasulu Mkoani Kigoma kupewa hifadhi.
Mkuu wa
wilaya ya Ngara Bw Constantine Kanyasu (Pichani akiongea na Wanahabari ) amesema
Raia hao wa Burundi wamesafirishwa jana na Shirika la Umoja wa Mataifa
linalowahudumia Wakimbizi, UNHCR kwa ajili ya kupewa Hifadhi kwenye Kambi ya
Nyarugusu
Amesema kuwa
kwa leo wamepokelewa Raia watano wa Burundi wanaoomba Hifadhi nchini ambao
wamehifadhiwa kwenye kituo cha Kuwapokelea katika Kijiji cha Kasange
Pichani ni Viongozi
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Kagera ilipofanya ukaguzi wa mpaka wake
wilayani Ngara na nchi jirani ya Burundi ili kujiridhisha na taarifa za kuingia
kwa wakimbizi kutoka nchini humo wanaodaiwa kukimbia maandamano ya kisiasa.
Katika hatua
nyingine, Baadhi ya Raia wa Burundi waliopewa Hifadhi kwenye Kambi ya Wakimbizi
ya Nyarugusu wilayani Kasulu Mkoani Kigoma wameishukuru Serikali ya Tanzania
kwa kuwapatia hifadhi hiyo.
Raia hao wa
Burundi wameziomba nchi nyingine kuiga mfano wa Ukarimu wa Watanzania na
Serikali yao kwa kuwa sio mara ya kwanza kuwapokea raia wa mataifa mengine na
kuwapa hifadhi na hivyo kuokoa maisha yao kutokana na machafuko yanayojitokeza
kwenye nchi zao.
Radio Kwizera
ikiwa Kambini Nyarugusu imeshuhudia Mabasi na Malori ya Shirika la Umoja wa
Mataifa linalowahudumia Wakimbizi, UNHCR yakiendelea kuwapeleka waomba hifadhi
hao Kambini humo wakitokea nchini Burundi.
Wakati huo
huo Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi amewasilisha Nyaraka zake kwa Tume ya Uchaguzi
nchini humo, CENI ili kujiandaa na Kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi
June mwaka huu 2015.
Rais Nkurunziza
amewasilisha Nyaraka hizo hapo jana pamoja na Faranga Milioni 15 za Burundi kwa
Tume hiyo ya Uchaguzi na kuthibitisha rasmi kuwa atawania Muhula wa Tatu wa
Urais kwenye Uchaguzi ujao
Hayo
yanajiri wakati Maandamano na ghasia za kupinga asiwanie Muhula wa Tatu wa
Uongozi kwenye uchaguzi ujao vikiendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Mwandishi wa
Radio Kwizera Mjini Bujumbura nchini Burundi amesema Mandamano na ghasia
zinazoendelea nchini humo zimesababisha vifo vya Watu 15 hadi sasa.
Source:-Radio
Kwizera FM.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni