Lowassa Hafai! Yes I said It - Sababu ya I
Watanzania wanajaribu kuaminishwa kuwa Lowassa anafaa kuwa Rais wa Tano
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wanaaminishwa kuwa ana maono ya
kiuongozi ambayo yakitumika yanaweza kulinasua taifa letu toka hapa
lilipo. Wanajaribu kuaminishwa kuwa Lowassa ni kiongozi bora ambaye
Watanzania wanapaswa kumwangalia kwa matumaini - ndio maana ya "Safari
ya Matumaini".
Wapo kati yetu ambao wameshazugika na pendekezo hilo na wamekuwa kama
waliorogwa hivi. Wapo baadhi yetu kwa muda wote wa uongozi wa Lowassa
(hasa baada ya kuwa Waziri Mkuu na baadaye) tuliona kile ambacho labda
kimefichika kwa wengi - Lowassa hafai.
Hii si hukumu juu ya utu wake, heshima au ubinadamu wake; ni hukumu juu
ya uongozi wake na maono yake kama kiongozi. Kumkataa Lowassa, maono
yake, uongozi wake na fikra zake siyo kumchukia yeye kama Mtanzania
mwenzetu au kama binadamu. Ni kuwa na tofauti naye na vile
anavyowakilisha kiasi kwamba tofauti hizo haziwezi kupatana
(irreconcilable differences).
Katika siasa ni lazima tuheshimu uwepo wa tofauti hizi na tuelewe ndio
msingi wa kutafuta viongozi bora zaidi au chama bora. Kwa kadiri yeye
atakavyojaribu kujiuza ndivyo na sisi wengine tutazidi kuonesha kuwa
hauziki au zaidi hanunuliki. Hii si chuki ni tofauti tu ya msingi
(fundamental difference).
Pendekezo langu linatokana na hili; kwamba zipo na zimedumu tofauti za
msingi kati ya maono ya baadhi yetu na maono ya mgombea huyu mtarajiwa
kutoka CCM. Tanzania haihitaji maono na uongozi wa Lowassa kwa sababu
nyingi tu; nitaanza na moja ya leo na nitaendelea kwenye mada hii hii
kila ninapopata nafasi hadi jina lake litakapotupwa na NEC na yeye
akaendelea kuwa Waziri Mkuu wa zamani.
Mara kwa mara baada ya sakata lake na katika jitihada za kujirudisha
katika umuhimu (relevance) Lowassa amekuwa akizungumzia mwelekeo wa sera
zake na kitu kitakachomuongoza. Aliamua kwenda kinyume na mwelekeo wa
serikali ya chama chake ambayo iliweka mkazo kwenye "Kilimo Kwanza";
yeye ameamua kuja na hoja ya "Elimu Kwanza".
Alielezea kupinga kwake hoja ya Kilimo Kwanza miaka michache nyuma
alipohojiwa katika kipindi cha Dakika45 (kinachorushwa na ITV).
Alinukuliwa kusema "
Mpango
huu wa Kilimo Kwanza umekosa nguvu kwa sababu kuanzishwa kwake
hakukuzingatia dhana ya ukombozi wa mwananchi wa kawaida. Tangu awali
ndani ya chama (CCM) nilieleza kuwa sitaunga mkono hoja hiyo mpaka
kuongezwe mashiko na kuwa Elimu Kabla ya Kilimo Kwanza"
Hoja hii ameirudia tena juzi kwenye mkutano wake na waandishi wa habari
ambao bila ya shaka wengi wamekuwa 'charmed' na wingu la umaarufu wa
Lowassa kiasi kwamba hakuna ambaye ameweza kumbana vizuri kwenye
maswali. Anasema endapo atachaguliwa basi ataelekeza nchi kwenye "elimu
kwanza"; kwamba hiki ndicho kipaumbele chake.
Ndio maana sisi wengine tunasema hafai; kwa sababu inaonekana siyo yeye
wala chama chake ambao wamelielewa vizuri tatizo linaloikabili Tanzania;
tatizo ambalo limeielekeza (orient) Tanzania kufuata njia ya Nigeria.
Kwamba tunaweza kabisa kutengeneza uchumi wenye nguvu lakini wa taifa
lenye umaskini uliokithiri, lisilo na usawa na la wasomi wasioweza
kulipeleka taifa mbele. Tutaishia kujisifia wingi wa wasomi ambao wengi
wataishia kwenda nje ya nchi kutafuta maisha. Taifa ambalo litakuwa
limegawanyika sana kama Nigeria - licha ya kuwa na wasomi wengi.
Lowassa inaonekana ameshindwa kuelewa au hataki kukubali kuwa tatizo kubwa la Tanzania ni la aina tatu:
1. Ufisadi
2. Ufisadi
3. Ufisadi
Lowassa hatopambana na ufisadi kwa uzito unaostahili kwani haoni kuelewa
kuwa ni tatizo la hatari zaidi kwa taifa "kuliko vita wakati wa amani"
kama alivyosema Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Kutokuelewa kuwa Ufisadi
ndiyo sekta haramu yenye nguvu zaidi katika nchi yetu ni kushindwa
kuelewa tatizo letu hasa ni nini. Ufisadi umepenya (permeate) kwenye
kila sekta nyingine zote (rasmi na zisizo rasmi). Umeathiri elimu, afya,
usalama, na hata umoja wa taifa. Kutokulielewa tatizo hili kwa mtu
anayetaka kugombea nafasi ya Urais (haijalishi anatokea chama gani) ni
kutokuelewa namna ya kukabiliana na changamoto nyingine zote.
Kwa sababu hii peke yake Lowassa na mgombea mwingine yeyote ambaye
haweki "ufisadi" kama ajenda yake ya kwanza na kubwa zaidi basi hafai.
Kwa sababu atatuzungusha kwenye madudu mengine yote isipokuwa kwenye
kumkoma nyani giledi.
Kikwete - kwa wanaokumbuka - alishabikiwa na wengi si kwa sababu ya "Ari
Mpya, Kasi Mpya na Nguvu Mpya" bali zaidi kwa kuwapa Watanzania
matumaini kuwa atashughulikia ufisadi vikali. Hotuba yake ya kulifungua
Bunge na ile ya Ngurdoto na zile ziara zake za kutembelea Wizara
ziliwafanya watu waamini kidogo kuwa hatimaye "kipele kimepata mkunaji".
Leo hii miaka tisa baadaye ripoti ya CAG imeonesha kidogo tu kuwa
tatizo hili la ufisadi halijapata mtatuzi ndani ya CCM na hata mtu
anayeshabikiwa sana kuwa ati anaweza kuwa Rais inaonekana tatizo hili
limempita kabisa.
Nikisema "hafai" simsingizii; nasema kilicho dhahiri;
I'm just stating the obvious.
Wanaomtaka Lowassa - wapenzi, mashabiki na waumini wake - watuambie vita
dhidi ya ufisadi ina umuhimu na uzito gani katika agenda za Lowassa.
Wakituambia kuwa "ni mojawapo" ya mambo atakayoyashughulikia tuendelee
kumkataa kwa sababu bado atakuwa hajaelewa tatizo letu hasa ni nini kama
taifa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni