Social Icons

Jumatano, 13 Mei 2015

Rais wa Burundi, Nkurunziza kuwasili leo Tanzania


 Rais wa Burundi Piel Nkuruziza leo atawasili nchini Tz ili kukutana na viongozi wa afirika mashariki kuona hatima ya mzozo unaoendelea nchin Burundi, je!!!, ww kama mudau wa haki zabinadamu unafikili nn ashauriwe Nkuruziza ili aache kung,ang,ania madaraka?.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ameitisha mkutano wa wakuu wenzake wa nchi hizo tano wa EAC, Jumatano hii, Mei 13, 2015, kujadili hali ilivyo katika nchi ya Burundi, kwa kadri nchi hiyo inavyojiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu Juni 26, mwaka huu.

Rais Kikwete ametangaza habari ya kuitisha mkutano huo wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) kuwaelezea matokeo ya mkutano wa wiki moja wa Jopo la Watu Mashuhuri Duniani linaloangalia jinsi dunia inavyoweza kukabiliana na majanga ya kiafya katika siku zijazo kufuatia balaa la ugonjwa wa Ebola katika Afrika Magharibi.

Rais Kikwete na wana-Jopo wenzake wamezungumza na waandishi wa habari jana, mjini New York, baada ya kuwa wamemaliza kikao cha kwanza cha Jopo lao lililoteuliwa na Katibu Mkuu wa UN, Mheshimiwa Ban Ki Moon, Aprili 2, mwaka huu, 2015, kupendekeza jinsi dunia inavyoweza kukabiliana na majanga ya kiafya, na hasa ya magonjwa ya mlipuko, katika siku zijazo kufuatia balaa na athari za ugonjwa wa Ebola katika Afrika Magharibi.

Ugonjwa wa Ebola umeua watu karibu 10,000 katika kipindi kifupi katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone.Hata kama ugonjwa huo ulijitokeza kwa mara ya kwanza mwaka 1976, karibu miaka 40 iliyopita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mpaka sasa ugonjwa huo hauna dawa inayojulikana dhahiri wala chanjo.

Katika maswali yaliyofuatia maelezo yake na ya wanajopo wenzake kuhusu kazi yao ya wiki moja, Rais Kikwete ameulizwa kuhusu hali ilivyo katika nchi ya Burundi, na Tanzania, kama jirani inachukua hatua gani kukabiliana na hali hiyo katika nchi jirani.

Rais Kikwete amesema kuwa mara baada ya mawaziri wa nchi za nje wa Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda kuwa wametembelea Burundi majuzi, kwa maelekezo yake, na kumaliza ziara yao kwa kujionea hali ilivyo katika nchi hiyo, ameamua kuitisha Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa EAC mjini Dar es Salaam Jumatano hii, Mei 13, 2015 ambako mawaziri hao watatoa ripoti yao ili ijadiliwe.

“Tumekubaliana kuwa sisi ndani ya EAC – Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi yenyewe tukutane Dar es Salaam, Jumatano, Mei 13, ili tujadiliane jinsi gani ya kuwasaidia ndugu zetu wa Burundi kuandaa uchaguzi wao kwa mafanikio wakihakikisha kuwa nchi yao inabakia na umoja, utulivu, usalama na amani bila misukosuko isiyokuwa na sababu,” Rais Kikwete amewaambia waandishi hao wa habari.

Ameongeza Rais Kikwete: “Baada ya hapo, tutaweza sasa kuwaelezea nyie waandishi wa habari kuhusu msimamo wa EAC na hata msimamo wa Tanzania kuhusu Burundi – tuwe na subira na tunaamini kuwa Burundi itaendelea kuwa ya utulivu na amani.”

Katika siku za karibuni kumekuwepo na hali ya mjadala mkali kuhusu maana halisi hasa ya Katiba ya Burundi, hususani katika kipengele kinachohusu vipindi vya kutumikia Urais. 


Baadhi wamekuwa wanadai kuwa kwa kutumikia miaka 10, Rais wa sasa, Mheshimiwa Pierre Nkurunziza amekamilisha mahitaji ya Kikatiba na wengine wakisema kuwa bado anayo haki ya kugombea kwa kipindi kimoja zaidi kwa sababu Rais amechaguliwa mara moja tu na wananchi.

Chama chake cha CNDD-FDD kimempitisha kuwa mgombea tena wa nafasi hiyo na wiki hii Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo imesema kuwa Rais Nkurunziza anayo haki ya Kikatiba kuwania nafasi hiyo kwa mara nyingine.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

9 Mei, 2015

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni